Mithali Sura 28
1
Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
2
Kwa sababu ya maasi ya nchi wakuu wake huwa wengi; Bali kwa wenye ufahamu na maarifa hali ya nchi hudumishwa
3
Mtu mhitaji awaoneaye maskini, Ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza chakula.
4
Wao waiachao sheria huwasifu waovu; Bali wao waishikao hushindana nao.
5
Watu wabaya hawaelewi na hukumu; Bali wamtafutao Bwana huelewa na yote.
6
Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri.
7
Yeye aishikaye sheria ni mwana mwenye hekima; Bali aliye rafiki wa walafi humwaibisha babaye.
8
Yeye azidishaye mali yake kwa riba na faida, Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.
9
Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo.
10
Kila mtu awapotezaye wenye haki katika njia mbaya, Ataanguka katika rima lake mwenyewe; Bali wakamilifu watarithi mema.
11
Mtu tajiri ana hekima machoni pake mwenyewe; Bali maskini mwenye ufahamu humchunguza sana.
12
Wenye haki washindapo, uko utukufu mwingi; Bali waovu waondokapo, watu hujificha.
13
Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.
14
Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote; Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara.
15
Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa; Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini.
16
Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana; Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake.
17
Aliyelemewa na damu ya mtu Atalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie.
18
Aendaye kwa unyofu ataokolewa; Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara.
19
Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha.
20
Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.
21
Kupendelea watu si kwema; Wala mtu kuasi kwa ajili ya kipande cha mkate.
22
Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri; Wala haufikiri uhitaji utakaomjilia.
23
Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali; Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake.
24
Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa; Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu.
25
Mwenye nafsi ya kutamani huchochea fitina; Bali amtumainiye Bwana atawandishwa.
26
Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga; Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa.
27
Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu; Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi.
28
Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.